Ndani kabisa ya kingo za Mto Oubangui katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuna sehemu ya kazi ya Jorres L., mwanajeshi mkongwe mwenye umri wa miaka 26 ambaye alipigana kwa miaka minne katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Kujumuishwa kwake katika maisha ya kiraia kuliwezekana kutokana na kazi kama mchimba mchanga.
Baada ya kuondoka kwenye kikundi chenye silaha, nilitafuta kazi kwa muda, lakini sikufanikiwa. Leo ninafanya kazi ya kuchimba mchanga na ninaweza kulipa kodi yangu. Mke wangu na mimi ni wazazi wa watoto sita, na ninaweza kuwategemeza kupitia kazi hii. Tangu wakati huo, nimekuwa nikijaribu kuwashawishi ndugu zangu ambao bado wanapenda kujiunga na sekta hii. Huwezi kuajiriwa katika nchi hii, lakini kazi hii inaniruhusu kujikimu.
Katika nchi ambayo viwanda vinakosekana, uchimbaji mchanga umekuwa chanzo cha ajira kwa vijana wengi wastaafu. Jeannet Kotisila anamiliki machimbo ya mchanga na ameajiri zaidi ya wanajeshi 150 wa zamani kama vibarua wa mchana.
“Kabla ya kufanya kazi ya uchimbaji mchanga, watu wengi wa jirani walikuwa hawana ajira. Lakini tangu wachukue kazi hii, maisha yao yameboreka, wameacha vitendo vyao vya zamani. Baadhi ya wafanyakazi hawa walikuwa wanamgambo Kazi hii iliwawezesha kuanza upya, kutoa maisha bora.”
Hakuna takwimu rasmi kuhusu idadi ya Waafrika ya Kati wanaofanya kazi katika machimbo ya mchanga, lakini profesa mmoja anaamini sekta hiyo inachangia pakubwa katika uchumi.
Walakini, kukosekana kwa udhibiti kunamaanisha kuwa wafanyikazi hawana dhamana ya afya, usalama na viwango vya mapato.
“Kwa upande wa manufaa, tayari ni jambo zuri kwamba wapiganaji hawa wa zamani wamekabidhi silaha zao na kufanya kazi ya kawaida,” anasisitiza Hermann Elokoua, profesa na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Bangui.
“Lakini ubaya ni kwamba watu hawa hawajajipanga, ambayo inamaanisha kuwa hawapati pesa za kutosha, pesa hizo hazitatosha kuwahudumia wakati wa ugonjwa.
Wakati mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, ukiendelea kupanuka, kazi ya mchimba mchanga ni muhimu zaidi kuliko hapo awali.
Watetezi wanaomba usimamizi bora wa machimbo ya mchanga ili wafanyakazi waweze kujikimu kimaisha.