Jukumu muhimu la bandari barani Afrika katika kuunganishwa na uchumi wa dunia haliwezi kupuuzwa. Rasilimali nyingi za bara hili hulifanya kuwa kivutio kikuu cha kununua baadhi ya madini muhimu na adimu zaidi ulimwenguni, mafuta, kobalti, bidhaa za kilimo.
Uuzaji wa bidhaa hizi nje umekuwa msingi kwa maisha ya uchumi wa kanda. Bandari hizi pia huchangia katika uundaji wa nafasi za kazi na uhamasishaji wa biashara za kikanda.
Swali linazuka kuhusu ni bandari gani muhimu zaidi barani. Mabilioni ya dola hutiririka kupitia bandari hizi, ambapo asilimia 90 ya bidhaa zote zinazouzwa barani humo, kulingana na Umoja wa Afrika, husafirishwa kwa njia ya bahari.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa na Bird TenX, wakala maalumu kwa masoko na mawasiliano, hizi hapa ni bandari 10 muhimu zaidi barani Afrika katika suala la wingi wa bidhaa zinazochakatwa:
1. Tanger Med – Iko kaskazini-mashariki mwa Tangier, Moroko, eneo hili la bandari ya viwanda linaweza kushughulikia makontena milioni 9 ya futi 20 (sawa na futi ishirini) na kusafirisha magari mapya milioni 1 kila mwaka. Pia hubeba abiria milioni 7 na malori 700,000.
2. Port Said – Bandari hii ya Misri iko kwenye mwisho wa kaskazini wa Mfereji wa Suez na inaweza kubeba hadi tani milioni 5 za makontena ya futi 20. Inachukuliwa kuwa bandari yenye shughuli nyingi zaidi nchini Misri.
3. Bandari ya Durban – Bandari kubwa zaidi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, iliyoko kwenye pwani ya mashariki ya Afrika Kusini, inaweza kuhudumia vitengo sawa vya futi ishirini (TEUs) milioni 2.9 na usafirishaji wa magari 600,000.
4. Lekki Deep Sea Port – bandari kuu ya Nigeria, ina uwezo wa kubeba kontena milioni 2.7 za futi 20. Iko katika Lagos, mji mkuu wa kiuchumi wa nchi.
5. Bandari ya Ngqura – Bandari hii muhimu iko kwenye pwani ya mashariki ya Afrika Kusini na iko ndani ya eneo maalum la kiuchumi. Ina uwezo wa TEU milioni 2.
6. Bandari ya Abidjan – Bandari hii ya Ivory Coast iliongeza maradufu uwezo wake wa uchakataji kwa kuongeza kituo cha pili cha kontena mwishoni mwa 2022. Sasa inaweza kuhudumia TEU milioni 2.5.
7. Bandari ya Casablanca – Iko karibu na Msikiti wa Hassan II huko Casablanca, bandari hii ya bandia inaweza kushughulikia TEU milioni 1.3 na tani milioni 21.3 za mizigo kwa mwaka.
8. Bandari ya Mombasa – Inayopewa jina la utani lango la kuingia Afrika Mashariki, bandari hii iliyoko nchini Kenya ina uwezo wa kubeba kontena milioni 1.65 kwa mwaka.
9. Bandari ya Doraleh – Iko nchini Djibouti, bandari hii ni upanuzi wa Bandari ya Djibouti na inaweza kushughulikia kontena milioni 1.65 kwa mwaka. Inaunganisha Ulaya, Mashariki ya Mbali, Ghuba ya Uajemi na Pembe ya Afrika.
10. Bandari ya Tema – Iko nchini Ghana, bandari hii inaweza kuhudumia TEU milioni 1.5 na ni mojawapo ya bandari muhimu zaidi katika pwani ya magharibi ya Afrika..
Bandari hizi zina jukumu muhimu katika kuwezesha biashara barani Afrika na kuchangia pakubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya kanda. Ni lango muhimu linalounganisha bara na uchumi wa dunia.