Mamlaka nchini Senegal zinakabiliwa na mzozo kuhusu tarehe ya kura nyingine ya urais, ambayo awali ilipangwa Februari lakini ikaahirishwa kwa miezi 10. Uamuzi huu ambao haujawahi kushuhudiwa unazua hisia kali, kikanda na kimataifa.
Rais Macky Sall alihalalisha kuahirishwa huku kwa kutaja mzozo wa uchaguzi kati ya Bunge na mfumo wa mahakama kuhusu baadhi ya wagombea. Hata hivyo, viongozi wa upinzani na wagombea walikataa hatua hiyo, wakiita “mapinduzi.”
Hali hiyo ilifikia hatua ya mzozo wakati wabunge kadhaa wa upinzani walipozuiwa kupiga kura na Bunge likapanga tarehe mpya ya kupiga kura ya Desemba. Hali hii ilizua hasira na lawama kutoka kwa watendaji wengi wa kisiasa. Hata hivyo, mamlaka ya Rais Sall yalikuwa yatakamilika Aprili 2.
“Tumesikitishwa na nchi yetu,” alisema Moustapha Kane, mwalimu katika mji mkuu wa Dakar, huku mvutano wa siku za hivi karibuni ukionekana kupungua. “Tulikuwa demokrasia kubwa. Sasa tuna hatari ya kuwa kicheko cha nchi nyingine.”
Kampeni za uchaguzi ziligubikwa na matukio mengi, kuanzia mapigano makali ambayo yalimfanya Sall kutangaza kwamba hatawania muhula wa tatu, hadi kunyimwa sifa za viongozi wawili wa upinzani na mamlaka kuu ya uchaguzi.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afŕika Maghaŕibi (ECOWAS), ambayo inakabiliwa na wimbi la mapinduzi katika kanda, inahimiza tabaka la kisiasa la Senegal “kuchukua hatua za haŕaka za kurejesha kalenda ya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Senegal.
Ni muhimu kutambua kwamba uchaguzi wa rais nchini Senegal haujawahi kuahirishwa hadi sasa. Katiba, hata hivyo, inalipa Baraza la Katiba, mamlaka ya juu zaidi ya uchaguzi, uwezo wa kurekebisha tarehe ya kupiga kura katika hali fulani, ikiwa ni pamoja na “kifo, kutokuwa na uwezo wa kudumu au kujiondoa” kwa wagombea.
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa pia ilielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Senegal, ikisisitiza haja ya kushauriana kwa upana kabla ya kufanya uamuzi wa kuahirisha uchaguzi.
Mgogoro huu unakuja wakati ECOWAS inakabiliwa na changamoto katika kudumisha mshikamano miongoni mwa wanachama wake. Nchi tatu zilizokumbwa na mapinduzi hivi majuzi zimeamua kujiondoa, zikiishutumu ECOWAS kwa vikwazo vya “kinyama” ili kukabiliana na unyakuzi wa kijeshi.
Kulingana na Oluwole Ojewale, mchambuzi wa Afŕika Maghaŕibi na Kati katika Taasisi inayolenga Afŕika ya Mafunzo ya Usalama, ECOWAS inapaswa kupunguza uingiliaji wake katika masuala ya kisiasa ya nchi wanachama au iimarishe jukumu lake la usimamizi.
“ECOWAS haiko sawa,” aeleza Bw. Ojewale. “Haiwezi kulaani mapinduzi ya kijeshi na kutishia kuingilia kati huku ikivumilia tabia ya kisiasa isiyowajibika katika mazingira mengine.”